Dodoma. Wabunge wamembana Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wakimtuhumu kuandaa taarifa za uongo, ufisadi na ubabaishaji kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa mwaka 2014/15, kuziwasilisha bungeni wakati hali halisi ikionyesha kuwa maeneo mengi nchini wananchi hawapati maji.
Bila kujali itikadi zao za kisiasa, wamesema hata
hotuba ya bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2015/16, haina jipya huku
Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje akiomba muongozo kwa Spika
ili waziri huyo afukuzwe bungeni akarekebishe takwimu zake.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya wizara hiyo ya
mwaka 2015/16 ambayo ilipitishwa jana jioni, Wenje alisema hotuba ya
waziri huyo imejaa ubabaishaji, uongo na ufisadi, “Mheshimiwa Spika
naona lingekuwa jambo jema kama waziri (Maghembe) afukuzwe humu ndani
ili aende kuandaa takwimu sahihi za wizara yake. Amelidanganya Bunge kwa
kutoa takwimu za uongo juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Jambo
hili halikubaliki katika dhana ya utawala bora.”
“Ni jambo la ajabu sana na ukiona uongo unatamkwa
wazi humu ndani ujue kuna hela zimepigwa. Inakuwaje unasema imetekelezwa
miradi 53 wakati iliyotekelezwa ni miwili tu,” alihoji Wenje.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy
alisema: “Waziri amepokea takwimu za uongo kabisa hizi ambazo hata
utafiti hazijafanyiwa. Hapa ni wazi kuwa fedha za wizara na halmashauri
zimeliwa.” Keissy alisema Sh1 bilioni zilizoahidiwa na Rais kuwa
zitakwenda katika jimbo hilo, zimefika Sh500 milioni tu na kati ya hizo
Sh8 milioni zimeshatafunwa na watumishi wa wizara hiyo.
“Nimekuwa nikitoa taarifa kwa Waziri Maghembe juu
ya wizi mkubwa wa fedha katika miradi ya maji katika wilaya ya Nkasi,
hasa eneo la Namanyere, Kirando, King’ombe na maeneo mengine lakini cha
ajabu Waziri anakuja hapa na takwimu kuwa maji yanatoka,”alisema kwa
kufoka. Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alitoa
mpya baada ya kusema kuwa anatamani kumcharaza bakora Profesa Maghembe
kutokana na kutoa taarifa za uongo bungeni kila mara.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Azza Hillal alisema,
“Hotuba ya waziri inasema vituo vya maji vinavyofanyakazi katika kijiji
cha Kagongwa ni 22 lakini ukweli ni kwamba vituo vilivyopo ni vinane
tu.”
Akizungumzia hayo, Mbunge wa Rungwe Magharibi
(CCM), Profesa David Mwakyusa alimtaka Profesa Maghembe kutoona aibu
kuweka kipaumbele katika kutekeleza miradi ya zamani badala ya kuomba
mipya ambayo haitekelezeki.
Kauli ya Kamati
Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imesema
Serikali haina nia ya dhati ya kupunguza tatizo la maji nchini kutokana
na kutoa asilimia 26 tu ya fedha za maendeleo za Bajeti ya Wizara ya
Maji mwaka 2014/15. Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, mwenyekiti wake
Profesa Peter Msolla alisema wizara hiyo iliidhinishiwa Sh488.8bilioni
kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini mpaka kufikia Machi mwaka huu
wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh129.3bilioni.
Kambi ya Upinzani
Akiwasilisha taarifa ya kambi ya upinzani ya
Wizara ya Maji kwa niaba ya waziri kivuli wa wizara hiyo, Magdalena
Sakaya, mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk alisema sekta ya maji
inakabiliwa na upungufu wa watumishi 6,901. Takwimu za wizara
zinaonyesha wataalam wanaohitajika ni 8,749 lakini waliopo ni 1,848,”
alisema.

No comments:
Post a Comment